TCD YAZINDUA JUKWAA LA MAJADILIANO YA VYAMA VYA SIASA ILALA
Na Mwandishi wetu, HPMedia, Dar es Salaam
Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania TCD Prof. Ibrahim Lipumba amesema kuwa mfumo wa Demokrasia imara ni ule unaofanya maamuzi ya kugusa maisha ya watu kuanzia ngazi ya chini huku akisistiza kuwa maamuzi hayo ni muhimu sana katika kuimarissha ustawi wa demokrasia nchini Tanzania.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa majukwaa ya majadiliano ya vyama vya siasa ngazi ya Wilaya kuhusu demokrasia ya vyama vingi ambapo amesema nchi yenye mfumo imara wa Demokrasi inafanya maamuzi yanayowahusu wananchi karibu na wananchi wenyewe na kusisitiza mwaka 2024 wadau wa siasa wanatarajia uchaguzi ulio huru na haki na unaozingatia misingi ya katiba.
Aidha, Prof Lipumba amehimiza umoja na mshikamano kwa viongozi vyama vya siasa ili nchi ya Tanzania iwe mfano katika mfumo wa demokrasia na uchaguzi unaozingatia katiba na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Zitto Kabwe amesema Rais Samia alitoa wito wa maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na ujenzi mpya wa Taifa ambapo amesema kupitia majadiliano hayo yatasaidia kujenga Taifa la watu ambao wamezungumza, wanasikilizana, wanaweza kutatua matatizo yai mezani na siyo barabarani na hivyo kujenga Taifa imara na la kidemokrasia.
"Naamini kwamba chini ya Uongozi wa TCD chini ya Mwenyekiti wake, Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti, Prof. Lipumba nchi hii itakaa kwenye meza ya majadiliano ya pamoja, tuwaombee kuelekea kwenye maridhiano na majadiliano." amesema Zitto.


Comments
Post a Comment