WAKILI MADELEKA AJIUNGA RASMI ACT WAZALENDO
Na Mwandishi wetu,
Wakili Peter Madeleka amejiunga rasmi na Chama Cha Act Wazalendo akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo amesema hatua hiyo ni kwenda kuunganisha nguvu katika upinzani.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa kadi na katiba ya Chama na Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho, amesema amekwenda upinzani kwa lengo la kusimamia na kuimarisha ili dola isiweze kuvidhoofisha.
Amasema kuwa, kudai demokrasia ya kweli katika nchi lazima kuwepo na njia mbalimbali ikiwemo kushiriki uchaguzi, kugombea, pia wakati mwingine kunakuwepo na vita kali ya kudai demokrasia hivyo amewataka Act Wazalendo kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Wakili Madeleka amesema vita kubwa ya vyama vya upinzani nchini ni CCM pamoja na Serikali yake kwani imekuwa ikibinya Demokrasia kwa vyama vya upinzani nakuvidhoofisha ili visishike dola.
"Tunaenda kushiriki uchaguzi ili kupima na kujiridhisha yale mabadiliko(Reforms)yanayosemwa yamefanywa na Serikali ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu kama ni kweli au la"amesema Wakili huyo msomi.
Awali akizungumza mbele ya wanachama na viongozi mbalimbali pamoja na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti Bara Is-haka Mchinjita amesema kuanzia leo Wakili Peter Madeleka ni mwanachama mpya ambaye atasaidiana na jopo la Wanasheria wa Chama hicho katika kutetea haki za kisiasa kupitia utaalamu wake wa sheria.
Amesema kuwa, Wakili Madeleka amekua msaada mkubwa wa kutetea haki za makundi yote katika jamii, huku akiacha historia nzuri ya kusimamia kesi ambazo zimekua zikitoka na matokeo mazuri.
Mchinjita amesema kuwa wakili Madeleka anauwezo mkubwa wa kuimarisha nguvu katika vyama vya upinzani na kutoa matumaini ya kufikia malengo ambayo chama kimejiwekea.


Comments
Post a Comment