Skip to main content

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR


Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii.

Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino .

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa.


"Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa," amesema Sinde.

Sinde amefafanua kuwa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti walikuwa watatu ambao ni Consolatha Modest Rwiza aliyepata kura 11, Juma Abas Mwingamno aliyepata kura 2, na Razalous Anosisye Mwakiposa aliyeibuka mshindi kwa kura 24.


Kwa upande wa nafasi ya Katibu Mkuu, wagombea walikuwa wawili ambao ni Athumani S. Gereza aliyepata kura 17 na Peppino Sudi Peppino aliyeshinda kwa kura 20.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Razalous Mwakiposa, ameushukuru umoja huo kwa kumchagua kuwa kiongozi wao na kusema kuwa, pamoja na mambo mengine, atahakikisha anapigania maslahi ya wenyeviti wa serikali za mitaa ili waweze kulipwa posho au mishahara inayokidhi mahitaji yao.

"Sisi ndio tunatumia muda mwingi ofisini kuwahudumia wananchi. Tunamuomba Mama (Rais Dkt. Samia) atukumbuke watoto wake tulipwe posho ama mshahara unaoweza kutusaidia kukidhi mahitaji yetu ili tufanye kazi kwa ufanisi mkubwa," amesema Mwakiposa, ambaye pia ni :Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Boko, Wilaya ya Kinondoni.


Akizungumzia suala la ulinzi na usalama, Mwakiposa amesema kuwa atashirikiana na wenyeviti wenzake kuhakikisha kunakuwepo vikundi vya ulinzi shirikishi katika kila mtaa, hali ambayo italeta utulivu na kuondoa vitendo vya uhalifu mkoani humo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Peppino Sudi Peppino, amesema kuwa yeye kama Mtendaji Mkuu wa umoja huo atashirikiana na mwenyekiti pamoja na wenyeviti wengine kufikia malengo waliyojiwekea.

Comments

Popular posts from this blog

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...