Na Ayra News.
Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji.
Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi.
Shushu alisema ushirikiano kati ya wataalamu wa Afro heal Group Limited na TIRDO umechangia kuongeza thamani ya mimea ya asili na kuiwezesha kampuni hiyo kuzalisha bidhaa zenye ubora wa juu.
Aliwahimiza vijana wenye mawazo ya ubunifu kutokata tamaa na kujitokeza TIRDO ili kupata ushauri na mwongozo wa kitaalamu, akisema hata kama hawatapokelewa moja kwa moja, wataelekezwa kwenye taasisi zinazoweza kuwasaidia kukuza bunifu zao.
Alisema ndoto ya Afro heal Group Limited ni kuwa miongoni mwa kampuni kubwa za Tanzania zinazozalisha dawa zinazotokana na mimea ya asili na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, aliwataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane 2026 kufika katika banda la Afro heal Group Limited kujifunza kuhusu teknolojia za uchakataji wa mimea, kujionea bidhaa zao na kupata elimu kuhusu fursa zinazotolewa na TIRDO kwa wabunifu wa Kitanzania.





Comments
Post a Comment