Skip to main content

DKT.MPANGO ATAKA AFRIKA KUBUNI NJIA BORA UENDELEZAJI RASILIMALI ZA NISHATI ILI KUKIDHI MAHITAJI




Asema upatikanaji wa Nishati Afrika bado ni mdogo kulinganisha na Mabara mengine

Asisitiza uendelezaji wa vyanzo vya Nishati uzingatie mustakabali wa vizazi vijavyo

Afungua Kongamano na Maonesho ya Petroli kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25)

Makamu wa Rais, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amesema kuwa matumizi ya nishati katika Bara la  Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara  bado ni madogo ikilinganishwa na maeneo mengine kama Bara la Amerika, Asia na Ulaya hivyo kuna umuhimu wa kubuni njia bora za kuzitumia rasilimali zilizopo ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia ili kuwawezesha wananchi kustawi kiuchumi na kijamii huku suala la utunzaji wa mazingira likizingatiwa.

Amesema hayo tarehe 5 Machi, 2025 wakati akifungua rasmi Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo litafanyika kwa muda wa Siku Tatu jijini Dar es Salaam.

“Katika kipindi ambacho maendeleo ya nishati endelevu yana mchango mkubwa katika mustakabali wa mazingira, uchumi na jamii zetu na katika kipindi ambacho Dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi bado tunahitaji  kutumia rasilimali zetu zilizopo, ikiwemo mafuta na gesi asilia lakini bila kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo ili kukidhi mahitaji ya kinishati.” Amesema Dkt. Mpango

Ameeleza kuwa, Afrika Mashariki imebarikiwa na rasilimali nyingi za nishati, ikiwemo mafuta na gesi asilia  ambapo  Tanzania imegundua gesi asilia, Uganda, Kenya na Sudan Kusini wamegundua mafuta, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wana gesi ya methane, huku Kenya na Tanzania zikiwa na rasilimali za nishati jotoardhi hivyo rasilimali hizo lazima  zitumike ili kupunguza pengo la nishati na kuharakisha maendeleo.

“Tunatambua kuwa ulimwengu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha madhara makubwa kama vile vipindi visivyotabirika vya mvua, mafuriko, mitetemeko ya ardhi na kuongezeka kwa joto. Tanzania, kama mataifa mengine, imejitolea kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa  ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kufanikisha azma ya kutozalisha hewa ya kaboni ifikapo mwaka 2050. Hata hivyo, tunapaswa kuweka uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na uendelevu wa vyanzo vyetu  kwa kutatua changamoto za leo huku tukijiandaa kwa changamoto za kesho.” Amesema Dkt. Mpango

Dkt. Mpango ameeleza kuwa, suala la kuhama kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi haliepukiki  kwani ni mkakati muhimu wa kupunguza uchafuzi wa mazingira duniani hata hivyo uwekezaji katika nishati hiyo unahitaji mtaji mkubwa na utaalamu wa hali ya juu ambapo inakadiriwa kuwa Afrika inahitaji kati ya Dola Trilioni 1 hadi 2 kufanikisha malengo ya  ya kuelekea kwenye nishati safi ifikapo mwaka 2030 hivyo kuna umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwa na ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.

Katika Mkutano huo wa EAPCE’25, Dkt, Mpango amesema kuwa anaamini Viongozi na Watalaam watabadilishana mawazo na uzoefu kuhusu kufungua fursa za uwekezaji katika nishati endelevu bila kusahau  nafasi ya rasilimali za mafuta katika upatikanaji wa nishati ya kutosha huku akisisitiza  ushirikiano wa kikanda kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, kadri uchumi unavyokua kwa kasi mahitaji ya nishati hasa Gesi Asilia yanaongezeka hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuendeleza miradi ya mkondo wa juu wa petroli kwa lengo la kugundua na kuendeleza  vyanzo vipya  vya rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia.

“ Nampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu  Hassan kwa jitihada zake za kuendeleza mkondo wa juu wa petroli ambapo chini ya uongozi wake uzalishaji wa  gesi umeimarika katika vitalu vya Songosongo na MnaziBay ambavyo ni muhimu katika uchumi wa gesi.”Amesema Dkt.Biteko

Dkt.Biteko ametaja baadhi ya mafanikio katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini kuwa ni pamoja na  uendelezaji wa gesi asilia iliyogunduliwa  katika  eneo la  Ntorya kitalu  cha Ruvuma kwa kutoa leseni uendelezaji wake kwa kampuni ya ARA Petroleum na kuongezeka kwa ushiriki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kitalu cha Mnazibay kutoka asilimia 20 hadi 40.

Naye Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Ruth Nankwabira Seitamo, ameeleza kuhusu umuhimu wa fedha zinazopatikana katika  Sekta ya Mafuta  na Gesi Asilia  kunufaisha Sekta nyingine  huku akitolea mfano kuwa nchini Uganda wameanzisha Mfuko wa Petroli ambao unahudumia sekta nyingine ikiwemo barabara, elimu, afya lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtu anafaidika na sekta husika.

Amesema sekta ya Mafuta na Gesi ni muhimu katika kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia hali itakayowezesha pia kupunguza uharibifu na misitu ambapo amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuwa kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Duniani.

Veronica Nduva, Katibu Mtendaji Jumuiya ya Afrika Mashariki amepongeza Tanzania kuendesha mkutano huo kwa mafanikio na kueleza kuwa unaendana na malengo ya Jumuiya ya EAC ya kuhakikisha kunakuwa na uendelezaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia unaozingatia utunzaji wa mazingira.

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...