Skip to main content

DKT.BITEKO AZINDUA MRADI UTAKAOWAKWAMUA VIJANA KIUCHUMI KATIKA MAENEO YANAYOPITIWA NA BOMBA LA MAFUTA GHAFI (EACOP)




Unahusisha kuongezea vijana ujuzi, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi

Ataka ujuzi unaotolewa kwa vijana uende sambamba na utoaji wa mitaji

Awaasa Vijana kuchangamkia fursa na kuwa waaminifu wanapopata nafasi

 Wanawake 6,130, Wanaume 4,905 na Makundi maalum 1,226 kufikiwa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua  Mpango wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana (YEE) ambao unagusa maeneo yanayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ikiwa ni jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa jamii zilizo karibu na miradi zinanufaika na miradi hiyo.

Akizindua mradi huo katika  Kijiji cha Bukombe, wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita tarehe 18 Agosti 2025, Dkt. Biteko amesema mradi huo wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ni moja ya miradi iliyopangwa kuwezeshwa na Kampuni ya EACOP kwa kipindi cha ujenzi na baada ya ujenzi ikiwa ni sehemu ya Uwajibikaji wa Kampuni hiyo kwa jamii. 

Amesema mradi huo umepangwa  kuwafikia zaidi ya vijana 12,261 ambapo miongoni mwao wanawake ni 6,130; wanaume 4,905 na makundi maalumu ni 1,226 katika awamu ya kwanza inayohusisha Mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga. 

" Tunapozindua mradi huu hatuna budi kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.

Viongozi wetu hawa kwa nia yao  ya dhati na moyo wa uzalendo wameuendeleza na  kuusimamia kikamilifu mradi huu wa EACOP ambao umefikia asilimia 65, tumefikia hapa sababu ya msukumo wao wa kutekeleza mradi huu " Amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa  tangu kuanza kwa mradi wa EACOP  mwaka 2022 hadi sasa,  jumla ya Watanzania 9,194 wamepata nafasi za kufanya kazi ndani ya mradi na hivyo kuwa fursa kwao ya kujipatia kipato, mwaka 2024 kampuni ilitoa mafunzo maalumu kwa Vijana 170 na kuwapatia kazi kwenye mradi, Vijana wengine 110 wapo katika masomo na wanatarajiwa kujumlishwa  pia katika Mradi huo pamoja na kutoa ufadhili wa Vijana 238 katika vyuo mbalimbali nchini. 

Amesema wananchi wanaopitiwa na miradi wanayo haki ya kunufaika na miradi lakini wana wajibu wa kulinda miundombinu ya mradi na kuufanya kuwa ni sehemu yao kwani unachangia pia kubadilisha maisha ya wananchi.

 Pia, Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya EACOP  na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) kwa kusimamia kwa ufanisi mradi huo huku akisisitiza kuwa, ili wananchi waone mradi huo ni sehemu yao lazima waone faida zake  hivyo miradi kama ya YEE inawapa chachu wananchi kulinda miundombinu ya EACOP kwa  wivu mkubwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, kampuni mbalimbali zinazotekeleza miradi kuhakikisha kuwa hawaweki mkazo  kwenye kuongeza ujuzi tu kwa wananchi bali wanawapatia mitaji ili waweze kufanya vizuri zaidi.

Aidha, amewaasa vijana kuchangamkia fursa zinazotokea kwenye miradi, wajitume, wawe waaminifu pale wanapopata fursa na kueleza kuwa Serikali itaendelea kuwatengenezea fursa  ili wajikwamue kiuchumi na kuleta maendeleo nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametengeneza mipango mikakati ya kuhakikisha vijana wanapewa fursa za ajira na mitaji kwenye maeneo mbalimbali ambapo mpango wa YEE ni kielelezo cha matokeo ya mipango hiyo.

Ameeleza kuwa, kumekuwa na programu mbalimbali ikiwemo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo kupitia programu hiyo zaidi ya shilingi trilioni tatu zilitolewa kwa Watanzania  takriban milioni 24 ikiwemo Wanawake,  Vijana na Makundi maalum kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi

Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa inayopitiwa na mradi wa EACOP amesema kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wananchi wa Geita wamenufaika nayo kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira za moja kwa moja na muda na mfupi pamoja na  mnyororo wa thamani kupitia biashara ya vyakula, mbogamboga, matunda n.k

Amesema Mpango wa  uwezeshaji wa vijana kiuchumi ni matunda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi hivyo mpango wa YEE unaongeza chachu hiyo ya utoaji elimu na ujuzi kwa wananchi wakiwemo vijana.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP wenye urefu wa km 1443 ni moja ya miradi 17 inayotekelezwa na Wizara ya Nishati ikiwemo mradi wa Julius Nyerere ( MW 2,115) ambao umekamilika, miradi ya umeme ya Ruhudji,  Rumakali na Malagarasi pamoja miradi mingine ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ukiwemo wa Eyasi Wembere.

Katika mradi wa EACOP amesema Serikali imechangia shilingi trilioni 1.12  ambazo ni hisa za Tanzania na kuna kampuni za kitanzania 200 ambazo zinafanya kazi mbalimbali katika mradi ambazo zitalipwa jumla ya shilingi trilioni 1.325 ikiwa ni moja ya matunda ya uwepo wa mradi huo nchini.

Akieleza sababu za kufanyika.kwa uzinduzi wa mradi wa YEE wiiayani Bukombe amesema kuwa Bukombe  kuna  kituo kikubwa zaidi cha kusukuma mafuta yatakayotoka nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga,   kuna kambi kubwa ya mradi wa EACOP na pia kilometa 20 za bomba hilo la mafuta zinapita katika eneo la Bukombe.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Mussa Makame  ameeleza kuwa, TPDC imeendelea kushirikiana na kampuni ya EACOP kuhakikisha kuwa mahitaji ya wananchi yanabainishwa na kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Ameeleza kuwa mahitaji yaliyoainishwa katika mradi wa YEE yaliandaliwa kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa kwa ngazi ya vijiji, Kata na Halmashauri zilizopo maeneo linapopita bomba la mafuta. 

Awali  Clare Haule - Meneja wa Uwekezaji na Uwajibikaji kwa Jamii katika kampuni ya EACOP alisema mradi wa YEE umeanzishwa kwa kutambua kwamba zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wa Tanzania ni vijana chini ya umri wa miaka 35. Hata hivyo, vijana wengi hasa katika maeneo ya vijijini wanakumbana na vikwazo vingi kama vile ukosefu wa ajira, ukosefu wa mafunzo ya ufundi stadi , na ugumu wa kupata mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara.

Alisema awamu ya kwanza ya Mradi wa YEE  utawawezesha kiuchumi vijana katika mikoa ya Geita, Kgera,Tabora, na Tanga na  mikoa inayobaki itanufaika katika awamu ya pili ambayo ni Singida, Shinyanga, Dodoma na Manyara ambapo vijana watapewa ujuzi  unaolingana na mahitaji ya soko, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi.

Aliongeza kuwa, Mradi wa YEE ni sehemu ya Sera ya Uendelevu ya EACOP, chini ya nguzo ya Vizazi Vijavyo, inayolenga kujenga uwezo wa vijana na kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi katika jamii zinazoguswa na mradi.

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...