Skip to main content

TMA YATOA UTABIRI WA MVUA ZA VULI OCTOBER HADI DISEMBA




Na Mwandishi wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, ikionya kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi ya nchi, huku baadhi ya maeneo machache yakitarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), ametoa taarifa hiyo leo Septemba 11, 2025 wakati akitangaza utabiri huo kwa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Ubungo Plaza.

"Vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha wa mvua vinatarajiwa kutawala hasa katika pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki," amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Kigoma, kabla ya kusambaa katika maeneo ya Simiyu na Shinyanga mwishoni mwa mwezi huo. Pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki zinatarajiwa kuanza kupata mvua wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba. Msimu huu wa mvua unatarajiwa kuisha Januari 2026.

Aidha, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa kuambatana na msimu huu, huku maeneo mengi yakikabiliwa na vipindi virefu vya ukavu na usambazaji wa mvua usioridhisha.

Amesema atharii mbalimbali zinaweza kujitokeza katika kipindi hicho ambapo katika kilimo kunatarajiwa kuwa na upungufu wa unyevunyevu katika udongo unaoweza kuathiri ukuaji wa mazao na kusababisha upungufu wa mavuno. Pia, magonjwa na wadudu waharibifu kama mchwa na panya wanaweza kuongezeka.

Katika sekta ya Maji na Nishati Dkt. Chang’a amesema, kupungua kwa kina cha maji katika mito na mabwawa kunatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji safi na hata uzalishaji wa umeme.

"Jamii inaweza kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama, huku hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na mbu ikitarajiwa kuongezeka." amesema.

Ameongeza kuwqla, Wafugaji wanaweza kukabiliwa na upungufu wa maji na malisho, hali inayoweza kusababisha migogoro ya ardhi huku pia baadhi ya maeneo yatakayopata mvua nyingi yanaweza kukumbwa na uharibifu wa barabara, mafuriko na kucheleweshwa kwa safari.

TMA imeendelea kuwashauri wakulima kuandaa mashamba kwa wakati na kutumia mbinu bora za kilimo ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza. Wafugaji wametakiwa kupanga matumizi bora ya malisho na maji, huku sekta za usafirishaji, afya, na mamlaka za serikali za mitaa zikihimizwa kuimarisha miundombinu na kuchukua tahadhari za mapema.

Aidha, amebainisha kuwa TMA inaendelea kutoa utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya. “Wilaya 86 zilizopo kwenye ukanda wa mvua mbili kwa mwaka, zitapatiwa utabiri wa kina wa maeneo madogo,” alisema.

Vilevile, wananchi wametakiwa kufuatilia kwa karibu utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, kila mwezi na tahadhari maalum inatolewa na TMA

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...