Skip to main content

NISHATI YAWASILISHA MIPANGO YA KIMKAKATI KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050





Ni katika kikao kazi na Tume ya Taifa ya Mipango.

Mradi wa usafirishaji umeme Chalinze–Dodoma ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele kufanikisha Dira 2050,

Wizara ya Nishati na Tume ya Mipango kushirikiana kwa karibu kusimamia miradi ya Nishati kufanikisha malengo ya Dira 2050.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amekutana na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango wakiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji – Menejimenti ya Utendaji na Tathmini, Dkt. Linda  Ezekiel kwa lengo la kujadili namna ambavyo Wizara na Taasisi zake zimejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati ya nishati inayochangia katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Msingi wa kikao hicho umetokana na  Sekta ya Nishati kuainishwa katika Dira 2050 kuwa ni moja ya  vichocheo vitano vitakavyoongeza kasi ya kufikia malengo ya Dira hiyo, ikielezwa kuwa Nishati ya uhakika ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha viwango vya maisha kwa kutoa fursa za ajira kwa maendeleo endelevu katika jamii.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma na  kuhusisha Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, 

Mha. Mramba amesema pande hizo mbili zimejipanga kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa miradi ya nishati ili kuhakikisha kuwa  inalingana na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo. 

“Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nishati ukiwemo mradi wa  kusafirisha umeme wa kV 400 wa Chalinze–Dodoma, ambao unatarajiwa kukamilika Juni 2026. Huu ni moja ya miradi  itakayoleta chachu ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Katavi, Kigoma na maeneo mengine ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme thabiti." Amesema Mhandisi Mramba

Amesema kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya umeme kutawezesha kutimiza moja ya shabaha katika Dira 2050 ambayo inaelekeza kuwa matumizi ya umeme yanapaswa kuongezeka na kufikia wastani wa Kwh 3,000 kwa kila mtu kwa mwaka.

“Tunataka kuwa Taifa lenye nishati ya uhakika, nafuu na safi kwa watanzania wote,  ili kutimiza lengo hili Serikali inawakaribisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya nishati  kwa kuwa mafanikio ya sekta hii yanategemea ushirikiano wa wadau wote. " Amesisitiza Mhandisi Mramba

Katika kikao hicho, Wizara pia iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Gesi Asilia na Mafuta,  Nishati Safi ya Kupikia, Umeme na Nishati Mbadala.

Kwa upande wake, Dkt. Linda  Ezekiel kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na Tume hiyo akisisitiza kuwa mwelekeo wa miradi iliyoainishwa katika kikao hicho inaendana na malengo ya Dira 2050.

Amesema Tume itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inachangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, kuboresha ustawi wa wananchi, na kulinda mazingira.

“DIRA ya 2050 inalenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi. Sekta ya Nishati ni mhimili wa kufanikisha hayo yote, tunapongeza jitihada za Wizara ya Nishati katika kuhakikisha nishati inakuwa injini ya maendeleo." Ameeleza Dkt. Ezekiel

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi yote inayogusa Sekta ya Nishati ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya  DIRA ya Maendeleo 2050 kwa ufanisi.

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...