Skip to main content

WAZIRI NDEJEMBI: WAKANDARASI WA UMEME WASIOFANYA VIZURI WASIPEWE MIRADI MINGINE





Apongeza mchango REA katika kufikisha asilimia 78.1 ya upatikanaji umeme vijijini.

Apongeza wakandarasi wazawa waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi; Ataka wapewe kazi zaidi.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wakandarasi ambao hawajafanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme inayosimamiwa na Wakala huo  kutopewa  kazi nyingine, ili kutokwamisha lengo la Serikali la kuwafikishia wananchi huduma ya umeme kwa wakati na kwa ufanisi.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo tarehe 22 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakandarasi wa miradi ya umeme pamoja na wadau wa miradi ya nishati vijijini.

 Kikao hicho kilienda sambamba na utoaji wa tuzo kwa wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini, ikiwemo waliokamilisha kazi mapema kabla ya muda wa mwisho wa mikataba yao.

"Umeme sasa si anasa, ni hitaji muhimu. Tunajenga Tanzania ambayo siyo tu ina umeme, bali inautumia umeme huo kwa tija katika kubadilisha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii. Umeme huu unaboresha mazingira ya kujifunzia mashuleni, unaimarisha utoaji wa huduma katika vituo vya afya, unachochea ukuaji wa biashara ndogo na kubwa, lakini pia ni kichocheo cha kufikia malengo ya Dira 2050," amesisitiza Mhe. Ndejembi

Katika kikao hicho ameipongeza REA kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, ambapo ufanisi huo umechangia kuongeza upatikanaji wa huduma ya umeme hadi kufikia asilimia 85.5 kitaifa na asilimia 78.1 katika maeneo ya vijijini, kutoka asilimia 2 wakati REA ilipoanzishwa mwaka 2007.

Vilevile, ameipongeza REA kwa kutimiza lengo la kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara, huku vitongoji 40,182 kati ya 64,359, sawa na asilimia 62.4, vikiwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

Akizungumzia wakandarasi waliopata tuzo kwa kutekeleza vizuri miradi yao, Waziri Ndejembi amewapongeza akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha uwezo mkubwa uliopo katika sekta ya nishati na inaweka msingi wa viwango vipya vya utendaji vinavyopaswa kuigwa na wadau wengine.

Pia amewapongeza wakandarasi wazawa waliotekeleza miradi yao kwa ufanisi na kupata tuzo, wakiwemo Derm Electric, SUMA JKT, Nakuroi na Sengerema, ambapo  amesisitiza kuwa kampuni hizo zipewe kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mingine ya umeme.

Katika kikao hicho, Waziri Ndejembi pia amewakumbusha wakandarasi kuzingatia ulipaji wa stahiki za wafanyakazi wanaowatumia katika utekelezaji wa miradi, kutumia vijana waliopo katika maeneo wanayofanyia kazi pamoja na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini na wananchi  kushiriki katika ulinzi wa miundombinu ya umeme.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kikao hicho ni cha pili kufanyika, kikiwa na lengo la kujenga utaratibu wa uwajibikaji, kuboresha ubora wa kazi na kutoa fursa ya kuwatambua wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na vitongojini ili kuendelea kuongeza ufanisi.

Amesema kwa sasa REA ina miradi mikubwa 13 inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku kukiwa na kandarasi 150 zinazolenga kupeleka umeme katika vitongoji takriban  17,000.

Ameeleza kuwa,  REA itaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa motisha, huku ikichukua hatua stahiki dhidi ya wale wasiotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba. 

Mhandisi Saidy ameshukuru viongozi wa Wizara ya Nishati kwa maelekezo na miongozo inayosaidia kusukuma utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wakala.

Pia, amewapongeza wakandarasi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi na kuwataka wale ambao hawakufanya vizuri katika tathmini iliyofanyika kuongeza juhudi. 

Aidha,  ametoa wito kwa wakandarasi wa Kitanzania kuendelea kujiimarisha kiufundi, kifedha na kiutawala ili kujenga kampuni imara zitakazoweza kutoa huduma hata nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amesema Bodi inajivunia kazi inayofanywa na Wakala, ikiwemo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara, huku utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme katika vitongoji ikiendelea na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.

Kutoka Wizara ya Nishati Waziri Ndejembi aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Bi. Anita Ishengoma

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...