Skip to main content

BOT YAFICHUA SABABU ZA KUENDELEA NA RIBA YA ASILIMIA 6.25





Na Ayra Newstz 

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi wa benki hiyo kuendelea na kiwango cha riba ya sera cha asilimia 6.25 unalenga kudhibiti mfumuko wa bei, kuhakikisha benki zinaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha kutoa mikopo na kuimarisha utulivu wa uchumi nchini.

Akizungumza alipotembelea banda la BOT katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Tutuba alisema kiwango hicho kilifikiwa baada ya tathmini ya hali ya uchumi wa ndani na mwenendo wa uchumi wa dunia.

Alisema BOT inaendelea kulenga kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya kiwango cha asilimia tatu hadi tano, huku ukwasi ukiendelea kuwepo katika mfumo wa benki ili kuwezesha ukuaji wa mikopo na shughuli za kiuchumi.

"Tunaamini kiwango hiki kitaendelea kuleta utulivu wa bei na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa kiwango kinachohitajika kuendesha shughuli za uchumi," alisema.

Tutuba alisema kipindi cha mavuno kinachokaribia kinatarajiwa kuongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania, hatua ambayo itawasaidia wakulima na wafanyabiashara kupata thamani stahiki ya mazao yao.

Mbali na sera ya fedha, alisema BOT inaendelea kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni za kusimamia mali za kidijitali (virtual assets), zikiwemo sarafu za kidijitali, ili kulinda watumiaji wa huduma hizo na kuzuia matumizi yake katika utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

Pia alisema mfumo wa Sema na BOT umeongeza ufanisi katika kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, huku juhudi zikiendelea kupanua wigo wa mfumo huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 60 ya BOT, Tutuba alisema taasisi hiyo imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha, mifumo ya malipo na utulivu wa uchumi, hali iliyochangia kuongeza imani ya wawekezaji na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na uchumi imara licha ya changamoto za kimataifa.

Comments

Popular posts from this blog

MWAKIPOSA MWENYEKITI MPYA WA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA DAR

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Boko Wilaya ya Kinondoni, Razalous Mwakiposa ameibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata kura 24 kati ya 37 zilizopigwa na wajumbe mapema leo hii. Uchaguzi huo umemalizika leo June 20, 2026ambapo  ulikua unahusisha nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu, ambapo Mwenyekiti ameshinda Razalous Mwakiposa huku Katibu Mkuu akiwa ni Peppino Sudi Peppino . Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi, Kambi Sinde, amesema kuwa Razalous Mwakiposa ameshinda kwa kupata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akishinda kwa kura 20 kati ya kura 37 zilizopigwa. "Uchaguzi umefanyika kwa uwazi na haki, kulikuwa na jumla ya wajumbe 40, lakini watatu walipata udhuru, hivyo, leo waliopiga kura ni wajumbe 37 na matokeo ni kwamba mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti amepata kura 24 kati ya kura 37 zilizopigwa, huku Katibu Mkuu akipata kura 20 kati ya kura 37 zilizop...

TIRDO YAVUNJA VIKWAZO VYA UBUNIFU, AFRO HEAL YAGEUZA MIMEA YA ASILI KUWA DAWA ZA KISASA

Na Ayra News.  Mashauri Enock Shushu, kutoka Afro heal Group Limited, amesema malezi ya ubunifu kupitia shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) yameiwezeshaa kampuni hiyo kubadili dawa za asili zilizokuwa zikitengenezwa kwa kutumia magome ya miti na kuzigeuza kuwa bidhaa za kisasa zinazokidhi viwango vya ubora na mahitaji utengenezaji soko. Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane 2026, Shushu alisema Afro healGroup Limited ni kampuni inayojihusisha na utafiti na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili, huku TIRDO ikiwa imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uwezo wao wa ubunifu na uzalishaji. Alisema kabla ya kujiunga na TIRDO, kampuni hiyo ilikuwa ikitengeneza dawa za asili katika mfumo wa magome, lakini baada ya kupata malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali watu kupitia taasisi hiyo, imefanikiwa kuziboresha na kuzalisha bidhaa za kisasa zinazorahisisha matumizi kwa wananchi. Shushu alisema ushirikiano kati ya wa...

VETA KAGERA WABUNI MTEGO KISASA WA KUVUNA SENENE

Ayra Nwestz  Chuo cha Veta mkoa wa Kagera VTC kimebuni mtambo wa kisasa wa kuvuna senene ambao unamuwezesha mvunaji kunapata senene wengi kwa wakati mmoja ambao wanakua salama. Akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima, katika maonyesho ya 47 ya biashara ya kimataifa, Mwalimu wa Kagera VTC, Elias Lucas Mayala, amesema chuo hicho kimebuni mtego huo una lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na mbinu za jadi za uvunaji. Mayala amesema kuwa mtanbo huo una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wakati wa uvunaji.  Aidha, amesema mtego huo una mfumo wa kuchuja senene wanapoingia na kuwatenganisha wadudu wadogo wadogo, ambao wanaweza kutumika kama chakula cha kuku badala ya kutupwa. Ameeleza kuwa tofauti na mbinu za zamani zinazoweza kuharibu miti na mazalia ya senene, mtego huo ni rafiki wa mazingira na umeundwa kwa namna inayorahisisha matumizi yake, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kusogezwa kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji...