Na Ayra Newstz
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeanzisha kampeni maalumu ya siku mbili ya kutoa huduma za uchunguzi, chanjo na elimu kuhusu ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis), huku ikionya kuwa wagonjwa wengi hufika hospitalini baada ya ugonjwa kufikia hatua za hatari.
Kampeni hiyo, inayofanyika kwa ushirikiano na Mega We Care Tanzania Limited,ambapo imeanza Julai 28 na itahitimishwa Julai 29, 2026 katika IDC Clinic iliyopo karibu na Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR) katikati ya Jiji la Dar es Salaam, huduma zote zinatolewa bila malipo kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ini wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Swaleh Kitabu Pazi, alisema hatua ya kupeleka huduma katikati ya jiji imelenga kuwafikia wananchi ambao mara nyingi hushindwa kufika hospitalini kutokana na majukumu yao ya kila siku.
Amesema kuwa, kliniki ya homa ya ini ya Muhimbili kwa sasa inawahudumia wagonjwa wapatao 5,000 waliosajiliwa, huku zaidi ya wagonjwa 100 wakifika kila siku kwa ajili ya matibabu na ufuatiliaji.
"Tunataka watu wajue hali zao mapema. Ugonjwa huu ukigundulika kwa wakati unaweza kudhibitiwa, lakini wengi wanafika hospitalini ukiwa tayari umeleta madhara makubwa," alisema Dkt. Pazi.
Alieleza kuwa homa ya ini aina ya B huambukizwa kupitia mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua, kujamiiana bila kinga, kuongezewa damu isiyo salama na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali vinavyotumika na watu zaidi ya mmoja.
Aidha, aliwataka wananchi kuachana na imani potofu kuhusu ugonjwa huo, akifafanua kuwa hauambukizwi kwa kushikana mikono, kukumbatiana, mate, jasho wala kuishi nyumba moja na mgonjwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Pazi, zaidi ya watu milioni 500 duniani wanaishi na maambukizi ya homa ya ini, huku takribani watu milioni 1.3 wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na madhara ya virusi vya homa ya ini aina ya B na C.
Amefafanua kuwa, pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, homa ya ini aina ya B inaweza kuzuilika kwa chanjo, wakati aina ya C inaweza kutibika endapo itagundulika mapema na mgonjwa kuanza matibabu kwa wakati.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Mega We Care Tanzania Limited, Mengi Ntasimba, amesema ushiriki wa kampuni hiyo katika kampeni hiyo ni sehemu ya mchango wake kwa jamii baada ya kuhudumu nchini kwa zaidi ya miongo miwili.
Ameongeza kuwa, kampuni imechangia vifaa vya uchunguzi, chanjo na dawa kwa watakaobainika kuwa na maambukizi, huku ikiendelea kushirikiana na taasisi za afya kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.
"Tunaamini kinga ndiyo msingi wa afya bora, kupitia kampeni hii tunataka wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kujua afya zao na kupata huduma kwa wakati," alisema Ntasimba.
Naye, Mfanyabiashara wa Kariakoo, Joseph Daniel Chengula, mkazi wa Kimara Mwisho, alisema alipata taarifa za kampeni hiyo kupitia mitandao ya kijamii na kuamua kufika kupatiwa huduma.
Amesema kuwa, huduma zinatolewa kwa utaratibu mzuri na bila usumbufu, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupima afya zao na kupata chanjo bila gharama.
Wataalamu wa afya wameendelea kusisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema, chanjo na matibabu ya haraka, wakieleza kuwa hatua hizo ndizo njia bora ya kupunguza maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa homa ya ini nchini.






Comments
Post a Comment