Na Mwandishi Wetu
Wakati changamoto ya ukosefu wa ajira ikiendelea kuwaathiri vijana wengi nchini, Zain Foundation imeanza kuonekana kuwa chanzo cha matumaini kwa wakazi wa Kata ya Keko, wilayani Temeke, baada ya kuanza kutoa ajira na kuendesha programu za kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza kuhusu shughuli za taasisi hiyo, Diwani wa Kata ya Keko na mmiliki wa kampuni ya Zain, Ismaili Said Amanzi, amesema tangu kuzinduliwa kwa Zain Foundation tayari vijana 10 wameajiriwa moja kwa moja, huku wengine wakinufaika kupitia programu mbalimbali za ukuzaji wa vipaji na ujasiriamali.
Amesema dhamira ya kuanzisha taasisi hiyo ni kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujiajiri na kuendesha maisha yao bila kutegemea wengine.
"Lengo letu ni kuwainua vijana wa Keko na kuwafanya wajitegemee kiuchumi. Tunataka watoke kwenye utegemezi na waweze kujenga maisha yao kupitia kazi na vipaji walivyonavyo," amesema.
Kwa mujibu wa Amanzi, Zain Foundation ilianza Keko kwa makusudi ili wananchi wa eneo hilo wawe wa kwanza kunufaika na kampuni yao ya nyumbani kabla ya huduma hizo kusambazwa katika maeneo mengine.
Amesema kwa sasa Keko ina matawi matano ya Zeini Foundation, ambapo kila tawi lina vijana 10, hivyo jumla ya vijana 50 tayari wanashiriki katika programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kiuchumi.
Mbali na kutoa ajira, amesema taasisi hiyo imeanza kuwasaidia vijana wanaotamani kuingia kwenye tasnia ya ubunifu kwa kuwapatia huduma za kurekodi maudhui bila malipo, huku ujenzi wa kituo cha mazoezi (gym) ukiendelea ili kukuza vipaji vya michezo na kuwahamasisha kushiriki shughuli halali za kujipatia kipato.
Amesema anaamini hatua hizo zitachangia kupunguza uhalifu miongoni mwa vijana na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Keko, Temeke na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia shughuli za kampuni yake, Amanzi amesema kampuni hiyo huzalisha zaidi ya bidhaa 150 za dawa za asili zinazolenga kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali za kiafya.
Amesema bidhaa hizo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili zinazopatikana Tanzania na kwamba kampuni inaendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa.
Amesema kuwa, kuhusu mafanikio ya kampuni hiyo, Amanzi amesema bidhaa za kampuni hiyo, tayari zinasambazwa katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Angola, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Namibia.
Amesema kutokana na mchango wake katika sekta ya dawa za asili, ametunukiwa tuzo ya heshima nchini Angola, ambako pia amealikwa mwezi Oktoba kufanya mazungumzo ya kufungua kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za kampuni hiyo.
"Nimefarijika kuona bidhaa zinazozalishwa Tanzania zinapata heshima katika masoko ya kimataifa. Hii inaonyesha vijana wa Tanzania wana uwezo wa kushindana na kuleta heshima kwa nchi yetu," amesema.
Amanzi amesema uzoefu wake katika biashara za kimataifa unaonyesha kuwa mataifa mengi yanaendelea kutumia dawa za asili kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo, kwa mtazamo wake, linapaswa kuwahamasisha Watanzania kuamini bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumzia kipindi cha mlipuko wa COVID-19, amesema Zain Company ilizalisha bidhaa za asili zilizotumiwa na baadhi ya wananchi katika kipindi hicho, huku akiishukuru Serikali ya wakati huo kwa kuhamasisha maendeleo ya tiba asili nchini.
Ametoa wito kwa Watanzania kuwa na uzalendo kwa kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini, akisema hatua hiyo itawasaidia wazalishaji wa ndani kupanua biashara zao na kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana.
"Tukiamini bidhaa zetu na kuwaunga mkono vijana wetu, watafika mbali, watafungua masoko mapya na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Tusikandamize juhudi za wazalishaji wa ndani, bali tushikamane kuwainua ili taifa letu linufaike," amesema.



Comments
Post a Comment