Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa wa saa 24 kuanzia saa 3:00 usiku wa Agosti 19, 2026, ikieleza kuwa baadhi ya maeneo nchini yanatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua na ngurumo, huku maeneo mengine yakitarajiwa kuwa na vipindi vya jua.
Kwa mujibu wa TMA, mikoa ya Kagera na Mara inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache pamoja na vipindi vya jua.
Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua nyepesi katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Aidha, Visiwa vya Unguja na Pemba, Kigoma, Tabora, Katavi, Manyara, Dodoma, Singida, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Pwani ikiwemo Mafia, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe na Songwe vinatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi pamoja na vipindi vya jua.
Mawimbi makubwa baharini
TMA imesema upepo wa Pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya hadi kilomita 30 kwa saa katika Pwani yote, ukitoka Kusini katika Pwani ya Kaskazini na Kusini Mashariki katika Pwani ya Kusini.
Katika hali ya bahari, mamlaka hiyo imesema mawimbi makubwa kiasi yanatarajiwa, hivyo watumiaji wa bahari wanashauriwa kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kabla na wakati wa safari.
Viwango vya joto
TMA pia imetoa viwango vya joto kwa baadhi ya miji nchini. Tabora inatarajiwa kuwa na joto la juu zaidi la nyuzi joto 31, ikifuatiwa na Kigoma, Mwanza na Zanzibar zenye nyuzi joto 30.
Dar es Salaam na Tanga zinatarajiwa kufikia nyuzi joto 29, Dodoma nyuzi joto 28, Iringa 26, Mbeya 24, huku Arusha na Njombe zikitarajiwa kufikia nyuzi joto 23.
Kwa upande wa joto la chini, Njombe inatarajiwa kuwa na kiwango cha chini zaidi cha nyuzi joto 8, ikifuatiwa na Mbeya nyuzi joto 11 na Iringa nyuzi joto 12.
TMA imesema kwa Ijumaa, Agosti 21, 2026, vipindi vya hali ya baridi vinatarajiwa kupungua katika maeneo mengi ya nchi.
Taarifa hiyo ni sehemu ya huduma za utabiri na tahadhari za mapema zinazotolewa na TMA kwa wananchi na sekta mbalimbali, ikiwemo usafiri wa baharini.

Comments
Post a Comment